
Kulinda chapa yako ni kulinda mustakabali wa kampuni yako. Katika makala haya, Sunday Ndamugoba anajibu maswali tata yanayowatatiza wafanyabiashara wengi kuhusu usajili wa nembo na alama za huduma nchini Tanzania.
1. Alama ya Biashara (Trademark) ni nini kisheria?
Ni alama inayotofautisha bidhaa za mfanyabiashara mmoja na mwingine. Inaweza kuwa jina, nembo, rangi, au hata mchanganyiko wa maneno yanayomfanya mteja akutambue sokoni.
2. Je, kuna tofauti gani kati ya “Trade Mark” na “Service Mark”?
Trade Mark hutumika kwenye bidhaa zinazoshikika (kama sabuni au nguo), wakati Service Mark hutumika kwenye huduma (kama ushauri wa kisheria, benki, au usafirishaji). Zote husajiliwa chini ya Sheria ya Alama za Biashara na Huduma (Sura ya 326).
3. Nani anaruhusiwa kusajili Alama ya Biashara BRELA?
Mtu binafsi, kampuni, kikundi cha watu, au taasisi yoyote inayofanya biashara au inayokusudia kuanza biashara inaweza kuomba usajili.
4. Je, kusajili kampuni BRELA kunatosha kulinda nembo yangu?
Hapana. Hili ni kosa kubwa. Kusajili jina la kampuni (Company Registration) hakukupi haki ya kumiliki nembo hiyo kama “Trademark”. Lazima ufanye usajili tofauti wa alama ya biashara ili kupata ulinzi kamili.
5. “Search” ni nini na kwa nini ni muhimu?
Kabla ya kuomba usajili, ni lazima kufanya utafiti (Search) kwenye mfumo wa BRELA ili kuona kama kuna alama nyingine inayofanana na yako. Hii inakuepusha na gharama za kukataliwa kwa maombi yako hapo baadaye.
6. Je, naweza kusajili nembo inayofanana na ya kampuni ya nje?
Hapana. Ukijaribu kusajili nembo inayofanana na kampuni inayojulikana duniani (kama Apple au Samsung), BRELA watakataa ombi lako kwa msingi wa “Well-known marks,” hata kama kampuni hiyo haijasajiliwa Tanzania.
7. Inachukua muda gani kupata hati ya usajili?
Mchakato huchukua kati ya miezi 6 hadi 9 kama hakuna pingamizi. Hii inahusisha uhakiki, utangazaji kwenye Gazeti la Alama za Biashara, na hatimaye kutoa cheti.
8. Nini maana ya “Classes” (Madaraja) ya usajili?
Alama za biashara zimegawanywa katika madaraja 45 (Nice Classification). Madaraja 1-34 ni ya bidhaa, na 35-45 ni ya huduma. Lazima uchague daraja sahihi kulingana na kile unachofanya.
9. Je, ninaweza kusajili alama moja katika madaraja mengi?
Ndiyo. Ikiwa kampuni yako inauza maji (Class 32) na pia inatoa huduma za usafiri (Class 39), utahitaji kusajili alama yako katika madaraja yote mawili ili kulindwa kote.
10. Alama iliyosajiliwa inadumu kwa muda gani?
Ulinzi wa kwanza unadumu kwa miaka 7. Baada ya hapo, unapaswa kuhuisha (renew) kila baada ya miaka 10. Ukichelewa, unahatarisha kupoteza haki ya kumiliki alama hiyo.
11. Nini faida ya kutumia alama ya ® dhidi ya ™?
- ™ (Trademark): Inatumika kuonyesha kuwa unadai umiliki wa alama hiyo lakini bado haijasajiliwa rasmi.
- ® (Registered): Inatumika TU pale ambapo usajili umekamilika na umepata cheti kutoka BRELA. Kutumia ® bila kusajili ni kosa la kjinai.
12. Je, ninaweza kuuza au kukodisha nembo yangu?
Ndiyo. Alama ya biashara ni mali (intellectual property). Unaweza kuuza (Assignment) au kutoa leseni kwa mtu mwingine kuitumia (Licensing) kwa makubaliano ya malipo.
13. Nifanye nini nikiona bidhaa feki zenye nembo yangu sokoni?
Kama umesajiliwa, unaweza kufungua shauri la kisheria la “Infringement”. Una haki ya kudai bidhaa hizo ziondolewe sokoni, ziharibiwe, na ulipwe fidia ya hasara uliyopata.
14. Je, rangi inaweza kusajiliwa kama Trademark?
Ndiyo, lakini ni vigumu kidogo. Lazima uthibitishe kuwa rangi hiyo imekuwa kielelezo cha kipekee cha biashara yako kiasi kwamba wateja wanakutambua kupitia rangi hiyo pekee.
15. “Opposition” (Pingamizi) ni nini?
Baada ya ombi lako kutangazwa kwenye gazeti la BRELA kwa siku 60, mtu yeyote anayehisi ombi lako litaingilia haki zake anaweza kuweka pingamizi la kisheria kuzuia usisajiliwe.
16. Je, ninaweza kusajili neno la kawaida kama “Chakula Bora”?
Hapana. Maneno ya jumla (generic terms) au yale yanayoelezea bidhaa moja kwa moja (descriptive terms) hayawezi kusajiliwa kama alama ya biashara kwa sababu kila mtu ana haki ya kuyatumia kuelezea bidhaa zake.
17. Je, usajili wa Tanzania unanilinda nchi za jirani kama Kenya?
Hapana. Sheria za alama za biashara ni za kitaifa. Ili kulindwa Kenya au Uganda, lazima usajili kupitia mifumo ya kikanda kama ARIPO au usajili moja kwa moja katika nchi hizo.
18. Je, naweza kubadilisha nembo yangu baada ya kuisajili?
Mabadiliko makubwa yanahitaji maombi mapya. Mabadiliko madogo sana yanaweza kufanyiwa marekebisho (alterations), lakini ni vyema kusajili nembo katika umbo lake la kudumu.
19. Nini kitatokea nisipohuisha (renew) usajili wangu?
Alama yako itaondolewa kwenye daftari la usajili (Removal for non-renewal). Hii inatoa mwanya kwa washindani wako kuisajili na kuitumia wao kisheria, na utapoteza haki ya kuwashtaki.
20. Kwa nini nitumie mwanasheria kama RIVE&Co. badala ya kufanya mwenyewe?
Mchakato wa BRELA una changamoto za kisheria, kuanzia uchaguzi wa madaraja, kujibu mapingamizi (objections), na kuhakikisha hati zako za kisheria zimeandaliwa kwa usahihi ili kuepuka kupoteza muda na fedha.
Mwandishi wa Makala hii ni Sunday Ndamugoba
Ikiwa una maswali zaidi au unahitaji kuanza mchakato wa kulinda brand yako leo, usisite kuwasiliana nami moja kwa moja:
- Mwandishi: Sunday Ndamugoba (Partner, RIVE&Co.)
- Barua Pepe: sunday@rive.co.tz
